Baraza la maimamu na wahubiri nchini CIPK, limezitaka pande mbili zinazozozana nchini Sudan Kusini kusitisha mgogoro huo.
Baraza hilo lilisema kuwa matamanio ya utawala yameyaponza maisha ya raia wengi wa taifa hilo.
Katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohamed Khalifa amesema kuwa wakati umefika kwa serikali za mataifa ya Afrika Mashariki kukemea kwa kauli moja mgogoro unaoendelea kushuhudiwa nchini Sudan Kusini.
Akizungumza siku ya Jumanne katika ofisi za baraza hilo mjini Mombasa, Khalifa alisema ni jambo la kusikitisha kuona umwagikaji wa damu unaondelea kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoshuhudiwa nchini humo.
“Ujumbe wetu kwa taifa jirani la Sudan Kusini ni kuwaomba kusikitisha umwagikaji wa damu wa wenyewe kwa wenyewe kwa kuua raia wasiokuwa na hatia,” alisema Khalifa.
Kauli ya baraza hilo inajiri wakati ambapo mji mkuu wa Juba unashuhudia mapigano baina ya vikosi tiifu kwa rais wa taifa hilo Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar ambapo kufikia sasa zaidi ya watu 200 wameripotiwa kuaga dunia.