Baraza Kuu la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, limeshutumu hatua ya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa Cord wakati wa maandamano ya siku ya Jumatatu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumanne, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa, alitaja vitendo hivyo kama vinavyoonyesha maadili mabaya sio tu katika idara ya usalama nchini, bali kwa taifa kwa jumla.

“Kanda iliyazagaa katika mitandao ya kijamii ikionesha polisi wakiwapiga waandamanaji imetazamwa kote duniani. Hio sio picha nzuri kwa taifa, kwa vile mataifa mengine yatatutambua kama taifa lisilolinda haki za wananchi wake,” alisema Khalifa.

Kiongozi huyo wa kidini hata hivyo aliwahimiza vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuzua vurugu.

Alitaja tukio la Jumatatu kama lililosheheni uhuni miongoni mwa vijana, hasa baada ya baadhi ya vijana kunaswa kwenye kanda za video wakipora mali za wenyewe.

“Wakati umefika kwa vijana kujitenga na viongozi wanaowapotosha na kuhatarisha maisha yao. Njia ni nyingi yza kuwasilisha maoni na malalamishi yetu. Sio lazima tuandamane,’’ aliongeza Khalifa.

Khalifa aidha alishikilia msimamo wake kuwa viongozi wa muungano wa Cord ni vyema watumie mbinu za amani ikiwemo kuandaa mazungumzo kuwasilisha mapendekezo yao, badala ya maandamano ya mara kwa mara ambayo huenda yakahatarisha usalama wa nchi.