Share news tips with us here at Hivisasa

Kituo cha kuwashughulikia watu wanaougua magonjwa sugu katika ukanda wa Pwani, Coast Hospice, kimewaomba wahisani kujitokeza na kusaidia kuchangisha fedha za kuendeleza huduma katika kituo hicho.

Kituo hicho cha kipekee katika eneo hilo la Pwani kilianza huduma zake mwaka wa 2011, na kimekuwa kikihudumia idadi kubwa ya watu wanaougua maradhi mbalimbali ikiwemo saratani.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne mjini humo, afisa anayehusika na maswala ya kifedha kituoni humo Bi Joyce Gitobu, alisema kuwa kituo hicho kinahitaji ushirikiano wa hali ya juu ili kiweze kutoa huduma kwa wakaazi.

“Tunaomba kampuni mbalimbali na hata watu binafsi wenye nia ya kusaidia wajitokeze na kutoa chochote walicho nacho ili watu wetu wasaidike.” alisema Bi Gitobu.

Afisa huyo alisema kuwa licha ya kwamba kituo hicho hujitahidi kuchangisha fedha, idadi ya wagonjwa wanaozuru kituo hicho huongezeka kila siku jambo linaloleta changamoto.

Takriban wagonjwa 100 hutembelea kituo hicho cha Coast Hospice kila mwezi kutafuta huduma mbalimbali ikiwemo dawa, matibabu, pamoja na ushauri.

Kituo hicho huwashughulikia wagonjwa ambao mara nyingi huwa wamekata tamaa ya maisha kutokana na kuugua maradhi hatari.

Kulingana na wauguzi wa kituo hicho, wamesaidia watu wengi ambao baadhi yao wamepona kabisa.

Kila mwaka kituo hicho huandaa zoezi la kuchangisha fedha za kusaidia huduma zake.

Kituo hicho kitaandaa tamasha la mchezo wa Golf eneo la Nyali mnamo Aprili 2, kwa lengo la kuchangisha pesa.

“Tunawahimiza watu wajitokeze katika hafla hiyo ambapo tuna matumaini ya kuchangisha pesa nyingi ili tuweze kubadilisha maisha ya watu wanaoteseka kutokana na magonjwa haya,” aliongeza Bi Gitobu.