Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika COMESA, linapania kujenga jengo la kibiashara nchini Uhabeshi litakalo tumika kama kitovu cha mataifa ya Bara la Afrika yanayotengeneza bidhaa zinazotokana na ngozi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa katika kongamano la muungano huo siku ya Jumatatu, Waziri wa Viwanda na Ustawi wa Biashara Adan Mohammed alisema kuwa jengo hilo litasaidia katika kutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kurembesha bidhaa za ngozi.

Bwana Adan alisema kuwa Bara la Afrika liko na raslimali nyingi ambazo zinaweza kutumika kukuza uchumi wa mataifa wanachama iwapo swala hilo litaanganziwa kikamilifu.

"Bara la Afrika lina raslimali za kutosha kuhakikisha kuwa tunakuza uchumi wetu na kuimarisha biashara. Mpango huu ambao tuko nao wa kujenga makavazi ama jengo la kibiashara litasaidia kuimarisha uchumi wetu Barani Afrika,” alisema Adan.

Waziri huyo alisema kuwa lengo lao kubwa ni kulifanya Bara zima la Afrika kuwa kigezo kikubwa cha kusafirisha bidhaa za ngozi hadi mataifa ya Magharibi.