Muungano wa Cord bado uko imara licha ya wengi kudai kuna malumbano na uhasama baina ya vinara wa muungano huo, haswa baada ya Raila Odinga kukosa kuhudhuria uzinduzi rasmi wa azma ya urais ya kiongozi wa FORD-Kenya Moses Wetangula ambaye ni mmoja wa vinara wa muungano huo.
Kulingana na mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir, mchemko unaoshuhudiwa katika muungano huo kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya muungano huo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017, ni ishara tosha kuwa muungano huo uko imara.
Akizungumza na wanahabari katika uwanja wa R.G Ngala wakati wa uzinduzi wa michuano ya Arosto Noma Inter Mitaa, Nassir amesema muungano huo utatumia njia ya maelewano na demokrasia kufikia uamuzi wa nani atakayepeperusha bendera ya muungano huo baina ya vinara wake watatu.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa mkataba baina ya viongozi hao watatu Raila Odinga, Moses Wetangula na Kalonzo Musyoka, Odinga bado anasalia mgombea mkuu wa muungano huo kwa mujibu wa mkataba wao hili likitokana na kuwa hakushinda urais katika uchaguzi mkuu uliopita.