Mbunge wa Mvita amesema kuwa muungano wa Cord bado uko imara licha ya wengi kudai kuna malumbano na uhasama baina ya vinara wa muungano huo, haswa baada ya Raila Odinga kukosa kuhudhuria uzinduzi rasmi wa azma ya urais ya kiongozi wa Ford-Kenya Moses Wetangula.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari katika uwanja wa R.G Ngala wakati wa uzinduzi wa michuano ya Arosto Noma Inter Mitaa siku ya Jumapili, Abdulswamad Nassir alisema kuwa mchemko unaoshuhudiwa katika muungano huo kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya muungano huo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017, ni ishara tosha kuwa muungano huo uko imara.

“Muungano wa Cord utatumia njia ya maelewano na demokrasia kufikia uamuzi wa nani atakayepeperusha bendera ya muungano huo baina ya vinara wake watatu,” alisema Nassir.

Mbunge huyo alisema kuwa kwa mujibu wa mkataba baina ya vinara hao watatu, Odinga bado ndiye anasalia mgombea mkuu wa muungano huo, kutokana na kuwa hakushinda urais katika uchaguzi mkuu uliopita.