Kiongozi wa Cord Raila Odinga amesema kuwa endapo serikali itamkamata Gavana wa Mombasa Hassan Joho, watavamia kituo cha polisi atakachokuwa amefungiwa na kumtoa.
Raila alitoa kauli hiyo kutokana na tangazo lililotolewa na Waziri wa Usalama wa ndani Joseph Nkaissery siku ya Jumanne, akimtaka Joho kurejesha bunduki yake kabla ya saa nane mchana, la sivyo akamatwe.
Akiongea mjini Nairobi siku ya Jumanne, Raila alisema kuwa Joho analindwa na sheria za katiba na kwamba hakuna mtu yeyote anayefaa kumtatiza.
“Hakuna mahali Joho ataenda na Nkaissery amevuka mstari mwekundu. Mkimkamata tutaenda hadi hapo kituoni na kumtoa,” alisema Raila.
Wakati huo huo, Joho alisema kuwa yuko imara na wala hana uoga wowote dhidi ya shutma anazowekelewa na kuongeza kwamba yeye ni kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.
“Sijafanya lolote na mimi siwezi kutishwa na mtu yeyote. Mimi nipo na kama mtu ananitaka anifuate,” alisema Joho.
Gavana Joho alikuwa mjini Nairobi pamoja na vinara wengine wa Cord kuhudhuria kuapishwa kwa mbunge mpya wa Malindi Willy Mtengo.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Seneta Moses Wetangula na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aliyeunga mkono maneno ya Raila na kusema kwamba Cord haitakubali dhulma anazofanyiwa Gavana Joho.