Kivumbi cha kisiasa kinatazamiwa wikendi hii huku vigogo wa kisiasa wakitarajiwa kuandaa mikutano tofauti ya kisiasa kujipigia debe.
CORD umetangaza kuwa utakuwa na mkutano wa hadhara katika eneo la Laini Saba, Kibera mkutano unaokinzana na ule wa maombi utakaoandaliwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na naibu wake, William Ruto katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
James Orengo na mwenzake, Johnson Muthama pamoja na mbunge wa Tongaren, Esieli Simiyu wamesema kuwa mkutano huo wa upinzani utalenga kushinikiza kutendewa haki kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/008 na pia mageuzi wanayotaka yafanyiwe tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.
“Tungependa kuwakaribisha wakenya wote kwenye mkutano wa hadhara utakaoandaliwa Jumamosi hii katika ukumbi wa Laini Saba, Kibera. Mkutano huu utakuwa ndi mwanzo wa kushinikiza kupatikana kwa haki kwa wahanga wa ghasia za baada ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na kufanyiwa mageuzi taasisi muhimu zinazosimamia Uchaguzi hapa nchin,’’ alisema Simiyu.
Muungano huo umesisitiza kwamba unasalia imara licha ya kile wanachotaja kama maombi ya mahasimu wao watengane ndiposa watumie fursa hiyo kusalia uongozini.
“Vyama tanzu chini ya CORD nikiwa na maana ya FORD-K, Wiper na ODM vinafahamu fika umuhimu wa umoja na viko tayari kufanya lolote ksualia imara hamna tashwishi kuhusiana na hilo. Kwa hivyo CORD tunasalia pamoja na tunawasihi wanaotaka tutengane watupe muda,” alieleza Simiyu.
Mkutano wa rais Kenyatta na naibu wake siku iyo hiyo unalenga kutoa shukrani kufuatia kuporomoka kwa kesi dhidi ya uhalifu wa kibindamu zilizokuwa zinawakabili katika Mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC.