Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa akina mama katika mrengo wa Jubilee kaunti ya Mombasa Shamsa Fadhil amekashfu hatua ya walimu kushiriki mgomo wakidai nyongeza ya mishahara akisema kwamba hatua hiyo inamkandamiza mwananchi wa mashinani.

Akizungumza katika mkutano wa mrengo huo mjini Mombasa siku ya Jumatano, Shamsa alisema kwamba akina mama wa kaunti hiyo wanaunga mkono kauli ya rais Uhuru Kenyatta ya kutowaongezea walimu mishahara kwani hatua hiyo itagharamu serikali na kuchangia hali ngumu ya maisha.

Shamsa alisema kwamba walimu wamechangia pakubwa matokea duni katika mitihani ya kitaifa kwa kuzembea majukumu yao, huku akihimiza serikali kutowalipa nyongeza hiyo.

“Walimu wanahitaji kuongezewa mshahara na wanafunzi wanazidi kuorodhesha matokeo duni katika mitihani ya kitaifa, hilo hatutakubaliana nalo hata kidogo,” alisema.

“Iwapo wanataka kuongezea pesa, basi mwanzo warudi shuleni wajitahidi tuone mtoto akifanya vyema kushinda yule wa shule ya kibinafsi ndio serikali iwape nyongeza wanayodai,” aliongezea Shamsa.

Aidha, amewataka viongozi wa mrengo wa Cord kukoma kuingiza siasa swala la mgomo wa walimu, kwani hatua hiyo huenda ikachangia mgogoro wa kisiasa na kuvuruga shughuli za masomo humu nchini.

“Viongozi wa mrengo wa Cord mwanzo wakome kuingiza siasa suala la mgomo wa walimu na kuacha vyama vya walimu kusitisha mgomo huo na walimu warudi shuleni,” aliongeza Shamsa.

Mapendekezo ya mwanahartakati huyo wa mswala ya kisiasa imejiri baada ya rais Uhuru Kenyatta kuhutubia waKenya na kusema kwamba serikali haiwezi kumudu gharama ya nyongeza ya walimu wanayodai.