Mrengo wa Cord unahofia kuwa huenda uchaguzi mdogo wa Malindi uliyopangwa kufanyika siku ya Jumatatu ukakumbwa na uwizi wa kura kutokana na maafisa wa usalama kuwa wachache katika vituo vya upigaji kura.
Akizungumza kwenye mkutano na wahabari siku ya Jumapili, Naibu Kinara wa chama cha ODM Hassan Joho alisema kuwa kuna madai kuwa chama cha Jubilee kina njama ya kuiba kura katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi ili kumpitisha mpinzani wao Philip Charo.
Joho alidai kuwa kuwepo kwa maafisa wachache wa tume hiyo pamoja na maafisa wa usalama ni ishara kuwa chama cha Jubilee kimejiandaa kufanya udanganyifu kutokana na kuwa Tume ya IEBC inasimamiwa na serikali, hivyo basi huenda uchaguzi huo ukakosa kuwa wa ukweli.
Joho alisema kuwa kama viongozi wa chama cha ODM, kamwe hawatakubali uchaguzi wa uongo, na kuwashinikiza maafisa wa tume hiyo kuwa makini ili kuzuia wizi wa kura na kuhakikisha uchaguzi huo ni wa huru na haki.
“Tunawaambia maafisa wa IEBC kuwa makini na uchaguzi wa Malindi pamoja na kuwachuguza vizuri wafuasi wa Jubilee kwani kuna madai kuwa wananjama ya kuiba kura. Hilo sisi hatutalikubali na tunachotaka ni uchaguzi wa huru na wazi,” alisema Joho.
Kampeni za uchaguzi huo wa Malindi zilikamilia siku ya Jumamosi na kupeana nafasi ya shughuli ya upigaji kura kufanyika siku ya Jumatatu.