Muungano wa upinzani wa Cord unataka Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet na Kamanda wa polisi Kaunti ya Nairobi Japheth Koome, kuchukuliwa hatua za kisheria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri kufuatia ripoti kuwa maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya wafuasi wa Cord wakati wa maandamano dhidi ya Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC, siku ya Jumatatu.

Cord imesisitiza kuwa sharti wawili hao wachunguzwe na kushtakiwa kwa kile walichokitaja kama kudhulimiwa kwa waandamanaji.

Muungano huo umemwandikia barua mkurugenzi wa mashtaka ya umma Bwana Keriako Tobiko wakitaka Boinet na Koome kushtakiwa kufuatia 'ukatili' wa polisi.

Wakizungumza katika afisi za ODM mjini Nairobi siku ya Alhamisi, Seneta wa Siaya James Orengo na Seneta wa Machakos Johnson Muthama, walimkashifu Waziri wa Usalama wa ndani Bwana Joseph Nkaissery kwa kile walichokitaja kama ukiukaji wa katiba.

Walimkosoa waziri huyo kwa kujihusisha na maswala ya polisi badala ya kubuni sera za Wizara ya usalama wa ndani.

"Inspekta mkuu wa polisi pamoja na kamanda wa polisi Kaunti ya Nairobi sharti washtakiwe kwa kukandamiza haki za waandamanaji,” alisema Orengo.

Viongozi hao walishikilia kuwa muungano huo utaendelea na maandamano yao ya kila Jumatatu kushinikiza kubanduliwa kwa IEBC.