Wabunge kutoka Pwani walioasi mrengo wa Cord na kuapa kufanya kazi na serikali ya Jubilee wamewataka wenzao wa upinzani kuipa serikali ya Jubilee muda ili kutekeleza ahadi zao kwa wakaazi wa Pwani.
Wakiongozwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mungaro na Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani, viongozi hao walisema kuwa mrengo wa Cord umeshindwa kutekeleza wajibu wake kama upinzani na badala yake wanatafuta kila njia ya kuweka siasa katika kila mradi wa Jubilee.
Viongozi hao walisema hayo walipoandaa mkutano wa harambee wa kuwasaidia waendeshaji bodaboda katika eneo la Lunga Lunga siku ya Jumapili.
Aidha, viongozi hao walisema kuwa wako tayari kugura Cord ili kuwania uongozi kupitia tiketi ya Jubilee katika uchaguzi mkuu ujao.