Mtaalam wa tiba asili amesema kuwa asilimia 60 ya wanaume ambao wamepoteza nguvu zao za kiume katika kanda wa Pwani ni watumizi wa dawa za kulevya na pombe.
Daktari Abdillahi Al Farsy, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la madaktari wa tiba asili nchini, amesema kwamba wanaume wengi hususan wale waliyo na umri wa miaka 40 kuendelea, hupoteza nguvu zao za kiume kutokana na matumizi ya vileo na pombe, utumizi wa sigara na vyakula visivyokuwa na virutubisho mwilini.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Dkt Farsy alisema kwamba viwango vya wanaume wanaopoteza nguvu zao za kiume katika ukanda wa Pwani vimeongezeka na ni sharti wanaume wabadili mitindo yao ya lishe, na kupunguza unywaji pombe na kisha watafute ushauri wa kimatibabu.
Mtaalam huyo wa afya eneo la Pwani amewataka wanaume kuthamini vyakula asili na kujitenga na vile vya mafuta mengi.
Daktari huyo alisema kuwa vyakula vya mafuta mengi na vile vya kisasa vimewafanya wanaume wengi kupoteza nguvu za kiume bila ya wao kutambua.
"Tunawashauri wanaume kuacha kutumia mihadatari na vileo kwani wengi wao huathirika katika hali yao ya nguvu za kiume,” alisema Dkt Farsy.
Dkt Farsy alisisitiza umuhimu wa wanaume kutafuta ushauri kuhusiana na afya ya uzazi ili waweze kuzidhibiti ndoa zao.