Wafugaji katika Kaunti ya Kisii wameombwa kutibu mifugo kufuatia Serikali kupunguza ada ya chanjo kwa kila mnyama.
Akiongea ofisini mwake siku ya Jumatatu, daktari wa mifugo katika Idara ya Mifugo Kaunti ya Kisii George Ondande aliwataka wakulima kuchukua nafasi hiyo kuwatibu wanyama wao kwa ada nafuu ya Sh30 kwa kila mnyama.
"Bei ya kutibu mifugo kwa sasa imepungua sana kulingana na ilivyokuwa hapo awali ambapo ni Sh30 kwa sasa kwa kila mnyama. Wakulima wanapaswa kuhakikisha wamewachanja mifugo yao angalau mara moja kwa mwaka," alishauri Daktari Ondande.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Madaktari wa mifugo katika Kaunti ya Kisii Omwoyo Moenga aliwashauri wafugaji kuchukua nafasi yao kutibu mifugo kwa kuwa Serikali imewajali kwa kupunguza ada ya huduma hiyo.
“Ningependa kuwaona wafugaji wakileta mifugo yao katika maeneo teule kwani bei sasa kwa kila mfugaji sio ghali ukizingatia hasara utapata iwapo mnyama wako atakuwa mgonjwa,” alisema Daktari Moenga.
Kwa upande mwingine Dkt. Ondande aliwataka wafugaji wote kusaka habari muhimu kutoka Idara ya Mifugo au kuuliza maswali yanayohusiana na mifugo kwa Mafisaa walioko karibu na Wilaya zao huku akiwasihi kushiriki makongamano ambayo huandaliwa na ofisi hizo.
Ushauri huu ulimetolewa huku ikibainika kuwa wafugaji wengi wamedinda kuchanja mifugo kwa kuhofia ada kubwa iliyokuwa ikitozwa hapo siku za mwanzo.