Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idara ya afya katika serikali ya Nyamira imeonywa dhidi ya kujenga vituo vya afya bila ya kuvipa vifaa na wafanyikazi wa kutosha. 

Akihutu kwenye wadi ya Bokeira siku ya Alhamisi alipokuwa akisaidia kuchangisha pesa za kugharamia matibabu ya mkazi mmoja, Dkt William Nyakiba alisema kuwa vituo vya afya vinaendelea kuongezeka kwenye kaunti ya Nyamira bila kuwepo wafanyikazi na vifaa vya kutosha, huku akiongezea kusema kuwa ni hasara kwa serikali ya kaunti hiyo kuendelea kujenga hospitali na zahanati mbalimbali bila ya kuhakikisha kuwa kuna vifaa vya kutosha kwenye zahanati hizo. 

"Wengi wenu hufikiri kuwa hospitali ni majengo tu, lakini lazima tuwe na wafanyikazi na vifaa vya kutosha ili hospitali hizo ziwe na maana, na hiyo sio hali huku Nyamira kwa kuwa serikali ya kaunti hii inaendelea kujenga zahanati bila ya kuwepo wafanyikazi na vifaa vya kutosha, swala ambalo halina faida kwetu," alisema Nyakiba. 

Nyakiba aidha aliongeza kwa kuiomba serikali ya kaunti hiyo kuhakikisha kuwa hospitali na zahanati zilizoko zina vifaa na wafanyikazi wa kutosha kabla ya kujenga vingine vipya kama njia ya kuwapa wanavijiji huduma za matibabu karibu na Nyumbani. 

"Ninaunga mkono kujengwa kwa vituo vya afya, lakini wacha serikali ya kaunti hii ihakikishe kwamba vile vilivyomo vina madawa, na wafanyikazi wa kutosha, na iwapo hilo halitazingatiwa basi huduma zetu za afya zitaendelea kudorora," alihoji Nyakiba. 

Nyakiba aidha aliisihi serikali ya kaunti kuihusisha hazina ya maendeleo bunge ili kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo vijijini haijirudii. 

"Nawasihi viongozi wa serikali ya kaunti hii kushauriana na hazina za maendeleo bunge kabla ya kutekeleza miradi mbalimbali kama njia mojawapo ya kuepusha visa ambapo miradi ya maendeleo hujirudii vijijini," alishauri Nyakiba.