Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Daktari anayesimamia ugonjwa wa kisukari katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii, Ongeri Angwenyi, amewahimiza wakaazi kutembelea hospitali kila miezi miwili ili kupimwa ugonjwa wa kisukari.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi nyingi ya wakaazi hawapendi kuzuru hospitali ili kupimwa na kujua hali zao haswa kwa ugonjwa wa kisukari.

Kulingana na daktari huyo, ugonjwa wa kisukari ni baadhi ya magonjwa yanayosababisha maafa mengi ulimwenguni. Aliwashauri wakaazi kutembelea hospitali ili kupimwa na kuanza kupata tiba ya mapema, iwapo watapatikana kuugua, jambo ambalo litapunguza makali ya ugonjwa huo.

Wakati huo huo, Angwenyi alisema kuwa wakazi 1,356 Kisii, wako katika orodha ya kupokea dawa za kupunguza makali, baada ya kugundulika kuwa tayari wameathiriwa na ugonjwa huo.

“Ni jambo la muhimu kila mtu ajue hali yake ya ugonjwa wa kisukari ndiposa nawahimiza nyote kutembelea hospitali kila baada ya miezi miwili ili kupimwa,” alisema Angwenyi.

Hata hivyo, alisema si rahisi kupata matibabu halisi ya ugonjwa wa kisukari, mbali kuna dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Ongeri aliwashauri wakaazi kupimwa ugonjwa wa kisukari na madaktari ambao wamehitimu, kwani kuna baadhi ya madkatari wanaweza kudanganya watu kuhusu ugonjwa huo.