Daraja muhimu inayounganisha mtaa wa Rainbow na Kaptembwa ilisombwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha alhamisi usiku.
Usafiri kati ya mitaa hiyo miwili imekatizwa huku wasafiri wakilazimika kwenda mwendo mrefu wakitafta barabara mbadala ya kutumia.
Watumizi wa barabara hii wamemtaka MCA wa eneo hilo bwana Daniel Ambale kuingilia kati na kukarabati daraja hilo ambalo ni la kipekee katika eneo hilo.
"Tumeteseka tangu mvua hii kunyesha na tunamwomba MCA kuikarabati barabara hii kwani anaishi kilomita chache toka mahala hapa. Kama wahudumu wa bodaboda inatulazimu kuwaacha wateja wetu hapa kwani pikipiki zetu haziwezi kuvuka katika ngambo ile nyingine," alidokeza Kevin Odongo ambaye ni mhudumu wa bodaboda katika eneo hilo.
Kwa upande wake Ambale ambaye ndiye MCA wa eneo hilo alisema amewasiliana na serikali ya kaunti kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuikarabati daraja hiyo.
"Nimeshawasiliana na ofisi husika katika kaunti yetu ya Nakuru na mikakati ya kurekebisha daraja hilo imependekezwa huku tukisubiri kazi rasmi kuanza kwa muda usio mrefu,"alisema
MCA huyo amewataka wananchi kuwa waangalifu hasa wakati huu wa mvua ili kuzuiya maporomoko.