Dereva mmoja wa gari ameponea kichapo kutoka kwa waendesha Bodaboda mjini Kisii baada ya kumgonga mmoja wa waendesha Bodaboda hao.
Dereva huyo wa kampuni ya Mabasi ya Otange alikuwa akielekea kwenye kituo cha magari ambapo inadaiwa kuwa alimgonga Zebedeo Nyabwanga ambaye alikuwa akitoka upande mwingine wa barabara inayoingia Ram Hospital na kumjeruhi vibaya kwenye muguu wake wa kulia.
Nyabwanga akiongea na Mwandishi huyu alidai kuwa dereva huyo alitoka upande wa chini wa barabara na hakumuonyesha ishara ya kupiga kona ndiposa kighafla alipata kumgonga kwa upande.
“Huyo dereva hakuonyesha signal yoyote kuwa alitaka kwenda upande wa kushoto ambapo mna steji ya magari. Nilishtukia tu amenigonga tayari,” alisema Nyabwanga huku akiwashtumu madereva wengine wa magari ambao amedai wamekuwa na mazoea ya kuwadharau waendeshaji Bodaboda wanapokuwa barabarani.
Matamshi yake yaliungwa mkono na mwenyekiti wa Bodaboda katika Kaunti ya Kisii Mike Onkundi ambaye alistaajabikia vitendo vya madereva kuwagonga wenye pikipiki mara kwa mara na wengi wao hutoroka wanaposababisha ajali kama hizo.
"Madereva wengi wa magari kubwa kubwa hasa Trailer na mabasi wana maringo na kudharau wenye magari ndogo ndogo na wenaoendesha pikipiki na kujiona juu ya sheria,” alihoji Onkundi huku akiahidi kupambana na utovu huo hadi mwisho na kuhakikisha kuwa heshima inadumishwa baina ya wenye Bodaboda na madereva wa magari.
Dereva huyo alitiwa mbaroni na bado anasaidia Polisi kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na ajali hiyo. Anazuiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Kisii Central pamoja na basi hilo kuzuiliwa.