Baraza kuu la waumini wa Kiislamu nchini SUPKEM limeonya vikali hatua ya baadhi ya watu kuingiza ukabila na misimamo ya kisiasa katika dini.
Hii inajiri baada ya Kadhi mkuu nchini kuishauri serikali kuwa siku ya Alhamisi iwe siku tengwa ya likizo kwa sikukuu ya Eid-ul-Fitri.
Akizungumza na meza ya habari ya Radio Rahma, Mwenyekiti wa SUPKEM Sheikh Muhdhar Khitamy alisema sio vyema dini kuingizwa siasa na akasema kuwa Kadhi huyo alitumia hekima mwafaka kutoa mwongozo huo.
"Alitumia hekma kuichagua siku ya Alhamisi kuwa ya likizo. Ila ukabila na misimamo ya kisiasa kuingizwa kwa dini sio jambo la busara," alisema Sheikh Khitamy.
Hivi majuzi, kamati ya Shuraa ilikuwa imemkosoa vikali Kadhi Mkuu kwa kutoa mwelekeo wa siku ya Eid wakimtaja kama afisa wa Mahakama na sio wa kidini.
"Tofauti za kikabila na kidhehebu hasipaswi kuwa kikwazo kwa waislamu haswa katika kipindi hiki cha saum," alieleza Sheikh Khitamy kwa mujibu wa meza ya Radio Rahma.