Mwakilishi wadi mteule Kisumu Faridah Salim ameshikilia msimamo wa kupigwa marufuku disco matanga kaunti hiyo.
Hii ni kutokana na kuwa hafla hiyo huchangia visa vya ubakaji kulingana na Salim.
Salim ashawasilisha hoja katika bunge la kaunti ya Kisumu akitaka sheria kuimarishwa zaidi kuwakabili wabakaji ikiwa ni pamoja na kushinikiza maslahi ya waathiriwa wa visa hivyo kushughulikiwa kwa haraka wanapopiga ripoti kwa polisi.
Amesema hafla za ‘Disco matanga’ hueneza ubakaji hasaa kupitia vinywaji, ulevi na kwa kushikwa kwa nguvu.
Mwakilishi huyu anasema mswaada huo unalenga kuona kuwa waathiriwa wa ubakaji hawalipi kupata fomu za P3 wanapopiga ripoti za kudhulumiwa kwa polisi na kwa idara ya mahakama kushugulikia kwa haraka kesi za ubakaji huku wahusika watenda visa hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria.
''Ni makosa na unyanyasaji kwa mwathiriwa wa ubakaji kutakiwa kulipa ili apate kupewa fomu ya P3 anapofika katika kituo cha polisi kupiga ripoti na hivyo mswaada kuhusu ubakaji niliyowasilisha kwenye bunge la kaunti ya Kisumu unalenga kuhakikisha haki za waathiriwa zinazingatiwa na wahusika watenda visa hivyo wanakabiliwa vikali kwa mujibu wa kisheria,'' akasisitiza Salim.
Farida amesema ni muhimu kwa haki za waathiriwa kuzingatiwa kwa uzito na ni jukumu ya sheria kuwalinda waathiriwa wa visa vya ubakaji kupitia taasisi mbali mbali.
Photo: