Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori hatimaye ameamua kuingilia kati na kutetea wafanyikazi wa kiwanda cha kutengeneza sukari cha Kiscol wanaodai kunyanyaswa.

Wafanyikazi katika kiwanda hicho kinachoongoza ukanda wa Pwani kwa utengenezaji wa sukari wanadai kulipwa malipo duni ikilinganishwa na kazi wanayofanya.

Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano mjini humo, mbunge huyo ameitaka usimamizi wa kiwanda hicho kuandaa kikao maalum na viongozi wa eneo hilo ili kutafuta suluhu.

“Watu wa Kiscol wanafaa kukaa chini na viongozi kujadili swala hili, hatuwezi kukubali wawekezaji kuendesha shughuli zake hapa wakati watu wetu hawafaidiki,” alisema Dori.

Mbali na madai ya malipo duni, wafanyikazi hao pia wanalalamikia mazingira duni ya kufanyia kazi jambo wanalodai linalemaza utendakazi.

Mbunge huyo ametaka kiwanda hicho kujali maslahi ya wafanyikazi wake akiongeza kwamba unyanyasaji wanaopitia unarudisha nyuma maendeleo ya kiwanda hicho.

Kwa upande wao wafanyikazi hao wametaja kutamaushwa na jinsi kiwanda hicho kinavyowashughulukia wafanyikazi wake huku baadhi wakisema kuwa wamekata tama.

“Wakati kiwanda hiki kilipoanzishwa hapa sisi tulikuwa na matumaini makubwa kwamba tungefaidi lakini tunachoona sasa ni dhulma ambapo hata baadhi yetu tunafikiria kutafuta kazi zingine,” alisema mfanyikazi mmoja.