Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wabunge kutoka maeneo bunge manne ya Kaunti ya Nyamira wameiomba tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC kuwachunguza kwa kina maafisa sita waliosimamishwa kazi kwa madai ya ufisadi.

Wakizungumza siku ya Jumapili katika hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kanisa ya kikatholiki ya Riakorongo iliyoko eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira, wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire waliomba tume ya EACC kuwachunguza maafisa waliosimamishwa kazi na gavana na kuwachukulia hatua kali ya serikali.

Wabunge hao pia waliiomba ofisi ya mfanyi hesabu ya utumizi wa pesa za serikali nchini kuchunguza kiasi cha pesa zilizopotea na jinzi zilipotea ili pesa hizo zirudishwe kwa hazina ya serikali ya Kaunti ya Nyamira.

Maafisa sita katika wizara mbalimbali katika kaunti ya Nyamira walihusishwa na madai ya ufisadi jambo ambalo lilimpelekea gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kuwasimamisha kazi baada ya bunge la kaunti hiyo kupitisha mswada kuzuia maafisa hao kuendelea kuhudumu katika nyadhifa zao.

Wabunge Timothy Bosire wa eneo bunge la Kitutu Masaba, James Gesami wa Mugirangio Magharibi, Charles Geni wa Borabu na Mwakilishi wa wanawake Alice Chae walifurahishwa na hatua ya Gavana Nyagarama ya kuwasimamisha kazi maafisa hao.

Wabunge hao walisema kuwa watafanya kazi na Gavana Nyagarama kwani ameanza kutekeleza kazi inavyostahili.