Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, imesema visa vya ufisadi nchini vimepungua kutoka asilimia 60 hadi asilimia 40 tangu tume hiyo ianze majukumu yake.
Afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Halakhe Waqo alisema visa vingi vya ufisadi vinahusishwa na wananchi wenyewe.
Waqo aliyasema haya huko Malindi kwenye warsha iliyojumuisha maafisa
kutoka idara tofauti za serikali, ambapo ameitetea tume hiyo na kusema ni jukumu la kila mkenya kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na sio tume hiyo pekee.
Hata hivyo amekiri kwamba ufisadi umerudisha nyumba taifa la Kenya.
Katika tathmini yake, tume hiyo imeeleza kwamba tayari kesi 363 za ufisadi zinazohusisha viongozi mbalimbali serikalini zimewasilishwa mahakamani.
Imesema kwamba kuwasilishwa kwa kesi hizo ni ishara wazi kuwa tume hiyo inajizatiti katika kukabiliana na ufisadi nchini.
EACC imedokeza kuwa tayari shilingi milioni 52 za sakata ya Chicken gate zitaregeshwa humu nchini kutoka Uingereza pamoja na shilingi milioni 525 zilizoporwa katika sakata ya Jersey.