Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu imezindua mipango mahususi inayonuiwa kuboresha sekta ya elimu katika kaunti hio.
Kwa mahojiano na ripota huyu, Waziri wa Elimu katika Kaunti hio Enock Mwigei amesema kwamba serikali hiyo imewaajiri takriban walimu 1,000 wa chekechea kwa njia ya kandarasi na wanaolipwa Sh10,000 kila mmoja kwa mwezi.
“Hii ni hatua ya kwanza ya Kukabiliana na uhaba wa walimu unaotokana na ukosefu wa fedha za kugharamia malipo yao,” alisema Mwigei.
Waziri huyo ameongeza kwamba, wamezindua ujenzi wa madarasa tisini yatakayoongeza idadi ya madarasa kuwa 180 ikijumulishwa na yale yaliyojengwa mwaka uliopita.
Amesema kwamba, ujenzi huo umezinduliwa ili kuhakikisha kwamba kila shule katika Kaunti hio ina angalau madarasa mitatu ya ECD.
Wakati huo huo idara hiyo imeanzisha mpango mwingine wa kuwapa vijana mafunzo katika vyuo anwai huku Kaunti hio ikiwa na vyuo anwai nane vilivyosajiliwa.
Waziri Mwigei alisisitiza umuhimu wa kuongeza nambari ya shule hizo vya anwai huku akisema kwamba tayari serikali ya Kaunti imetoa shilingi milioni ishirini na saba mwaka uliopita na itatoa milioni ishirini na mbili mwaka huu ili kuendeleza mpango wa kusajili shule zingine ili kila Kaunti ndogo iwe na angalau shule mbili ya anwai.