Mkurugenzi wa nishati mbadala katika Tume ya kudhibiti kawi ya ERC Robert Oimeke, amesema kuwa tume hiyo itafunga vituo vya mafuta vinavyoendesha shughuli zao kinyume cha sharia katika eneo la Pwani.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiongea katika kongamano lililowahusisha wadau katika sekta ya kawi nchini, lililofanyika mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Oimeke alisema kwamba kumekuwepo na mchipuko wa vituo vya mafuta visivyo halali, hasa katika Kaunti ya Mombasa, na tayari tume ya ERC inaendeleza mchakato wa kuvifunga vituo hivyo.

Aidha, alisema kwamba japo baadhi ya wafanyibiashara wamekabidhiwa leseni na tume hiyo kutekeleza biashara hiyo ya mafuta ya petroli, baadhi yao wameanzisha vituo hivyo katika maeneo ya makaazi au katika maeneo yasiyofaa.

Mkurugenzi huyo alisema kwamba pia wanalenga wahandisi wanaojenga vituo hivyo kinyume cha sheria na kuupuza masharti ya tume hiyo.

"Kama tume tunachunguza vituo vya mafuta vinavyoendesha shughuli zao kinyume cha sheria. Tutazifunga kwa vile kwa sasa sheria iko wazi kuwa kila kampuni lazima isajiliwe kwa tume ya ERC,” alisema Oimeke.