Kuvunjika kwa ndoa ya Susumila, msanii tajika kutoka Mombasa, kumeendelea kuzua hisia mseto miongoni mwa wakaazi pamoja na wanamuziki kutoka Pwani.
Wengi wamesema kuwa hilo ni jambo la kustaajabisha ikizingatiwa kuwa Susumila alifunga pingu za maisha mnamo Oktoba 22, 2015, katika harusi iliyohudhuriwa na wasanii mbalimbali kutoka Mombasa.
Escobar, msanii maarufu kutoka Mombasa ambaye hapo awali alikuwa katika kundi moja la muziki na Susumila kabla ya kikundi hicho kusambaratika, alisema kuwa licha ya tofauti zao za kimuziki, hakufurahia jambo hilo.
Alisema kuwa wasanii wengi wameweza kupotezwa na umaarufu, jambo ambalo alisema huwasababisha kutelekeza familia zao.
Mwanamuziki huyo alisema kuwa muziki ni kama kazi yoyote ile na ni muhimu kwa wasanii kuwa na ndoa na familia imara.
“Msaani anapokuwa na familia, yeye huheshimiwa zaidi na hata kuonekana na wengi kama mtu wa maana,” alisema Escobar.
Aidha, alisema kuwa licha ya kuibuka madai kuwa wawili hao wamekuwa wakitofautiana kwa muda kabla ya kuafikia uamuzi huo, Susumila anapaswa kufanya juu chini kuinusuru ndoa hiyo.