Spika wa Bunge la Seneti Ekwee Ethuro ameahidi kuundwa kwa sheria zitakazokuza biashara na ajira nchini ili kumaliza umaskini.
Ethuro amesisitiza kuwa hatua hiyo itaimarisha uchumi wa taifa mara dufu.
Aidha, ameongeza kuwa janga la umasikini litazikwa katika kaburi la sahau iwapo sheria hizo zitapitishwa na kufuatwa.
Haya yanajiri baada ya wakuu wa muungano wa sekta za binafsi nchini KEPSA, pamoja na maseneta kukubaliana kushirikiana kubuni ajira.
Hii ni mojawapo ya mikakati iliyowekwa kufanikisha ruwaza ya mwaka 2030.
Mwenyekiti wa muungano wa KEPSA, Dennis Awori, alisema kuwa baadhi ya mikakati waliyoweka ni pamoja na seneti kupitisha miswada ya sheria ambayo itafanya uendeshaji wa biashara kuwa rahisi.
Awori alisema kuwa maseneta wanahitajika kufikiria namna ya kupunguza kodi za biashara na kupunguza mfumko wa bei nchini.
Aidha, alisema kuwa kuwepo kwa utulivu wa kisiasa nchini ni muhimu kwa ustawi wa biashara, hivyo basi iko haja ya kuwa na amani nchini tufikapo kwenye uchaguzi mwakani.
Ethuro alikuwa akizungumza siku ya Ijumaa kwenye kikao na wakuu wa muungano wa sekta za binafsi nchini KEPSA, pamoja na maseneta katika hoteli moja jijini Mombasa.