Zaidi ya familia elfu moja ambazo zimekuwa zikiishi katika msitu wa Baraget wilayani Kuresoi kinyume cha sheria zimepewa makataa ya wiki moja kuuhama msitu huo la sivyo wafurushwe kwa nguvu.
Akiongoza maafisa wa serikali ambao walizuru msitu huo, naibu kamshna wa jimbo Silas Gatobu amesema wananchi wamenyakua msitu huo ambao ni chemchemi inayotegemewa na wakazi wengi katika kaunti mbali mbali.
Amesema lengo la serikali ni kuhifadhi msitu wa Baraget kama ilivyofanyika katika msitu wa Mau huku akiuliza wananchi hao kuhama kwa hiari kabla ya serikali kuchukua hatua.
Afisa mkuu wa misitu katika eneo hilo Peter Nyambati amesema wakazi hao walioingia msituni bila idhini lazima watoke ama wahamishwe kwa lazima.
Hata hivyo wakazi hao wamesema wameishi katika msitu huo kwa zaidi ya miaka 16 huku wakiuliza serikali kuwapa makao mbadala kabla ya kuwafurusha.