Zaidi ya wakazi 500 katika kijiji cha Kajiwe eneo la Rabai wanalalamikia kuvunjiwa nyumba zao na bwenyenye mmoja anayedaiwa kunyakua ardhi yao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea na wanahabari siku ya Jumapili, wakazi hao waliyo familia ya aliyekuwa mganga wa kienyeji maaruuf kama Mzee Kajiwe, ilisema kuwa ardhi hiyo ni yao tangu jadi, lakini cha kustajabisha bwenyenye huyo alivamia makazi ya wakazi hao na kubomoa nyumba zao bila ya kuwaarifu.

Familia hiyo, ikiongozwa na mke wa marehemu Mzee Kajiwe Mama Salama alishtumu hatua hiyo na kuitaka serikali kuingilia kati ili kusaidia kupata ardhi yao ambayo bwenyenye huyo anaendelea kubomoa nyumba za familia hiyo.

“Tunashanganzwa na bwenyennye huyo, alituma watu na matinga kubomoa nyumba zetu hata makaburi ya marehemu pia yanavunjwa, tafadhali serikali tunaiomba kuingilia kati swala hili na kuturudishia ardhi hiyo,” alieleza Mama Salama.

Naye Mwakilishi wa Wadi ya Rabai-Kisurutini Kenga Mupe alikashfu hatua hiyo akidai kuwa bwenyenye huyo angefaa kutoa notisi kabla ya kuvunja nyumba za wakazi, hata kama aliuziwa ardhi hiyo kwa njia ya siri ama na baadhi ya maafisa wa umma.

“Sisi tunakashfu vikali hatua hii na tunasema kuwa lazima tutaelekea mahakamani kwa sababu ardhi hii sisi tunajua ni ardhi ya marehemu Mzee Kajiwe na familia yake bado iko hapa, hata makaburi pia bado yako, sasa mbona huyu jamaa anachukua hatua ya kuwafurushwa wakaazi hiyo hatutakubali,” alisema Mupe.