Wizara ya ardhi imeulizwa kutatua mzozo wa ardhi unaotokota kati ya usimamizi wa shule ya upili ya Mukinyai na familia sita kutoka eneo hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Familia hizo zinadai wasimamizi wa shule wanakusudia kuwatimua kutoka kwa mashamba yao.

Familia hizo ambazo zina hatimiliki ya mashamba hayo zimesema mwanzilishi wa shule hiyo ambaye kwa sasa ni mmoja wa wanakamati, alisimamia ujenzi wa shule kwenye ardhi iliyotengewa chuo anuwai (polytechnic) huku shamba la ekali 14 lililokusudiwa kujengwa shule ya pili likibaki bila kutumiwa.

Wakazi hao wakiongozwa na Rev Samuel Wahugu wamesema ramani ya shamba lote la Mukinyai inadhibitisha kwamba shule hiyo ilijengwa kwenye ardhi isiyofaa jambo ambalo linazua ugomvi kati ya wenyeji na wasimamizi wa shule.

Wahugu amesema itakuwa ukiukaji mkubwa wa haki zao za kimsingi iwapo wasimamizi wa shule pamoja na mawakala wao wataharibu mali yao ikizingatiwa kwamba mahakama imetoa onyo kwa watakao ingilia ama kubomoa vifaa kwenye mashamba ya walalamishi.

Bi Cecilia Wangari, John Karau na Samuel Ngige Mungai wamesema wanamatumaini kwamba idara ya mahakama pamoja na wizara ya ardhi itaingilia kati na kutatua mgogoro huo wakihofia huenda kukazuka mapingano iwapo mzozo huo hautatatuliwa mara moja.

Wakazi hao wamesema wamekuwa wakitatizika huku wakilazimika kusafiri mwendo mrefu baada ya barabara waliokuwa wakitumia kufungwa na wasimamizi wa shule jambo ambalo linatatiza usafiri.

Aidha kila familia imeonyesha hatimiliki za mashamba hayo pamoja na stakabadhi zingine wakisema wameishi katika mashamba hayo tangu miaka ya sabini.