Familia moja katika eneo la Kwa Ndung’u viungani mwa mji wa Molo imeachwa bila makao baada ya ndimi kali za moto kuzuka na kuteketeza nyumba yao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Juhudi za wakaazi kudhibiti makali ya moto huo ziliambulia patupu, huku kila kitu kikigeuzwa majivu kwenye mkasa huo.

Mmiliki wa boma hilo Mbugua Mwangi amesema anakadiria hasara kubwa baada ya kupoteza kila kitu kwenye moto huo, ambao chanzo chake kinadhaniwa kuwa hitilafu za nyaya za solar zinazosambaza nguvu za umeme hadi kwenye betri.

Mwangi, ambaye ni baba wa watoto wanne ameiomba serikali pamoja na wahisani kumsaidia, ili aweze kurejelea maisha ya kawaida.

Aidha, Wakaazi wilayani Molo wanaendelea kushinikiza serikali ya kaunti ya Nakuru pamoja na hazina ya CDF kufadhili ununuzi wa zana za kukabiliana na majanga ya moto, baada ya kuona wananchi wamekuwa wakipoteza mali yenye thamani kubwa kwenye ndimi za moto.

Visa sawa na hivyo vimekuwa vikiongezeka katika eneo hilo, huku wakaazi wakilalamikia utepetevu wa maafisa wa polisi kukabiliana na majanga hayo.