Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Familia moja kutoka wilaya ya Molo Kaunti ya Nakuru imeitaka wizara ya ardhi na tume ya ardhi kitaifa kuchunguza na kuwachukulia hatua kali za kisheria mabwenyenye  ambao wamenyakua shamba lao la ekari 10 lililo eneo la Mai Mahiu.

Jamaa wa familia hiyo wakiongozwa na Samwel Ng’ang’a, Jackson Njoroge na Peter Waweru wamesema wameeleza kuhangaika kwao baada ya kupata shamba lao limenyakuliwa na mwekezaji wa kibinafsi ambaye baadaye aliuzia kundi moja la watu ardhi hiyo bila ya ufahamu wa familia hiyo.

Wamesema juhudi zao za kupata haki zimeambulia patupu, huku walionyakua shamba hilo wakitembelea afisi mbali mbali kama njia moja ya kuhujumu utekelezwaji wa haki.

“Tulipata hatimiliki ya shamba hilo mwaka wa 1971, na tungali ndio wamiliki wa shamba hilo,” alisema Peter Waweru.

Kulingana na Waweru, afisa mmoja wa C.I.D, ambaye alidai kwamba anachunguza swala hilo, alichukua stakabadhi zao za umiliki wa shamba hilo miezi mitano iliyopita, na hadi sasa afisa huyo hajawarudishia stakabadhi zao.

"Afisa huyo wa CID hajaturudishia hati miliki, licha ya kwamba alisema atachunguza unyakuzi uliodaiwa upo kwa siku tatu peke yake," alisema mzee huyo.

Kwa sasa familia hiyo imeitaka serikali, kupitia wizara ya ardhi pamoja na mkuu wa C.I.D, kuchunguza kisa hicho.

Visa vya unyakuzi wa ardhi katika kaunti ya Nakuru vimeripotiwa kuongezeka, huku wengi wa wanaopoteza ardhi zao mikononi mwa wanyakuzi wakiwa ni wazee ama familia zinazozozana.