Familia ya mwanamke aliyefariki baada ya kupigwa risasi wakati wa makabiliano baina ya wahudumu wa bodaboda na polisi huko Likoni inaomba msaada wa kusafirisha mwili huo hadi Kisumu kwa mazishi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Familia hiyo inayoishi eneo la Mrika, Likoni, imesema imebaki katika njia panda kwani licha ya kukosa fedha za kusafirisha mwili huo hadi nyumbani Kisumu, bado pia wanakabiliwa na deni la hospitali.

Akizungumza na mwandishi huyu nyumbani kwao siku ya Jumatatu, kaka mdogo wa marehemu, Kelvin Ochieng, alisema tangu mkasa huo ulipotokea hakuna msaada waliopata.

“Imekuwa mzigo kwetu kwa sababu nyumbani ni mbali na kusafirisha mwili kunahitaji pesa nyingi. Hakuna mahali tumepata msaada hadi kufikia sasa,” alisema Ochieng.

Ochieng alisema wanahitaji zaidi ya shilingi 200, 000 kulipia gharama ya hospitali pamoja na kusafirisha mwili huo.

Mamake mwendazake Bi Jenifer Atieno alisema familia yake haina haja ya kupewa fidia yoyote kutokana na kifo cha binti yake, kwani tangu tukio hilo lilipofanyika, polisi wamekuwa wakiwazungusha bila kuwasaidia.

“Polisi wanasema sio wao waliomuua binti yangu. Mimi sitaki kufanya kesi wala malipo yoyote. Kile ninachotaka ni msaada nikamzike mwanangu,” alisema Atieno.

Mwili wa marehemu Emilly Anyango bado umehifadhiwa katika Hospitali ya Coast General, huku familia hiyo ikiendelea kutafuta msaada.

Kwa upande wake, polisi anayefanya uchunguzi kuhusu kisa hicho amesema bado hawajapata ushahidi wa kubaini iwapo ni polisi ndio waliohusika na mauaji hayo.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu afisini mwake katika Kituo cha polisi cha Likoni siku ya Jumatatu, Inspekta Joseph Omwanda alisema bado wanendelea na uchunguzi.

Marehemu ambaye amewaacha watoto wawili, alikuwa mhudumu wa duka la dawa na M-Pesa.