Familia moja katika mtaa wa Matumaini viungani mwa mji wa Molo wameitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria machifu wawili ambao wanashukiwa kuuza shamba la walalamishi kwa mwekezaji wa kibinafsi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Familia ya Thomas Omundi mwenye umri wa miaka 75 imeshutumu machifu wa kata ya Matumaini wilayani Molo kwa kushirikiana na Thomas Oeri - mwekezaji wa kibinafsi ambaye anawafurusha kwenye ardhi yao ambapo wameishi kwa zaidi ya miaka 32.

Wamesema wanaishi kwa hofu kwani hivi majuzi, baba yao alipigwa na kujeruhiwa vibaya na kundi la vijana ambao walitumwa kuwafurusha kwa nguvu kutoka shamba lao.

Wenyeji hao ambao wana hati miliki ya shamba hilo lenye ekari mbili na nusu pia wana stakabadhi kutoka kwa wizara ya ardhi ambazo zinadhibitisha umiliki huo.

Wanasema wamezika jamaa zao watatu katika shamba hilo ikiwemo ndugu yao aliyefariki 2002, dada yao 2006, na mama yao 2010 na kwa sasa wanahofu kwani maafisa wa serikali badala ya kuwasaidia baadhi yao wanapuuza kilio chao.

Wamesema licha ya wakili Onkoba Omariba kuandikia wahusika wote barua na kuwaonya kuacha kusumbua na kuharibu mali ya familia hiyo, bado mmiliki huyo bandia pamoja na mawakala wake wanaendelea kuwavamia.

Wamesema wahusika hao wameharibu mali ya thamani kubwa ikiwemo nyumba pamoja na kuzika kisima chao cha maji na kuacha familia hiyo ikihangaika.

Machifu hao ambao walionekena kulaumu familia hiyo kwa kufichulia wanahabari masahibu yao walidinda kunena na wanahabari kuhusu madai yaliyotolewa.