Familia ya mzee Fidels Nyang’au kutoka lokesheni ya Keumbu, Kaunti ya kisii, imeomba serikali ya kaunti hiyo kuwasaidia kumtatafuta mwanao kwa jina Christopher Onderi, aliyekuwa katika chuo cha Garissa kulichoshabuliwa siku ya alhamisi.
Hii ni baada ya kukosekana kati ya wale waliouawa, na wale wengine 31 waliosafirishwa Kisii siku ya Jumapili.
Wakiongea nyumbani mwake hii leo, Jumanne, Nyang’au, ambaye ni babake Onderi, amesema waliongea na mwanaye kupitia njia ya simu siku ya Alhamisi asubuhi wakati mwanae alimwambia kwamba alikuwa mahala pabaya, na kumwambia wamwombee kama familia na tangu siku hiyo hajawahi wasiliana nao.
“Naomba serikali inisaidie kumtafuta mwanangu kwa kufanya uchunguzi kama yuko hai au aliuawa bora nijue yuko wapi, kwani amekosekana hadi sasa,” alisema Nyang’au.
Wanakijiji cha Nyamware wanaendelea kushikwa na butwaa baada ya kukosekana kwa kijana huyo aliyekuwa akisomea tahaluma ya ualimu, kwani matumaini yao yalikuwa kwa kijana huyo na kusema wamekumbwa na giza kisichoelezeka.
“Kakangu alikuwa mpole na ndiye tuliweka tegemeo letu, maana babangu amekuwa akisumbuka kumsomesha kwa kufanya ukulima ili kuhakikisha kuwa kakangu amesoma, tunaomba serikali ifanye juhudi za kuchunguza na kutujulisha kama yuko hai ama amekufa,” alisema Shadrack Nyakundi, kakake mwasiriwa.
Ni siku Mbili tu zimepita baada ya wanafunzi 31 walionusurika kuletwa kutoka Garissa, na serikali ya kaunti ya kisii imeahidi kuzisaidia familia zile wanao waliathiriwa katika shambulizi lililotokea Garissa.