Familia moja eneo la Bamburi kaunti ya Mombasa inaitaka wizara ya elimu nchini kuingilia kati ili iweze kupata haki baada ya mtoto wao kufariki katika ajali alipokuwa shuleni.
Marehemu Mohamed Hussein mwenye umri wa miaka 17 alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Mwagogho kaunti ya Taita Taveta.
Inadaiwa kundi la wanafunzi lilitoka nje ya shule kufanya mazoezi ya kukimbia, lakini walipokuwa wanarudi shuleni Mohamed na mwenzake wakaabiri gari kuelekea nyumbani kwa rafiki yake kabla gari hilo kuhusika katika ajali.
Kijana huyo alifariki papo hapo huku mwenzake akipata majeraha mabaya, katika ajali hiyo iliyotokea tarehe 12 mwezi Machi mwaka huu.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini humo, babake marehemu Hussein Abdallah alisema kuwa anatafuta haki kwani shule hiyo iliwaruhusu wanafunzi kutoka nje bila kuwa na mwalimu husika.
“Mimi nataka nipate haki yangu kama mzazi kwa sababu mtoto anapokuwa shuleni najua yuko chini ya usimamizi wa waalimu,” alisema Hussein.
Mzazi huyo anasema mwalimu mkuu wa shule hiyo amepuuza swala hilo na wala hakuna maelezo yoyote aliyopewa.
Aidha Hussein alidokeza kuwa mkurugenzi mkuu wa elimu kaunti hiyo ya Taita Taveta Jonathan Nyamai alikuwa ameahidi kuwasaidia lakini punde baada ya mazishi ya kijana huyo akakatisha mawasiliano.
“Mkurugenzi wa elimu saa hii nikimpigia simu hataki kushika, alikuwa amesema atahakikisha tunapata haki lakini hakuna msaada tena,” aliongeza.
Sasa amewasilisha kilio chake kwa mashirika mbalimbali ya kutetea haki huku pia akitoa wito kwa wadau wa elimu akiwemo waziri wa elimu Fred Matiang kuingilia kati.
Kwa upande wake Francis Auma, afisa kutoka shirika la Haki Afrika alisema kuwa wamemuandikia barua mkurugenzi huyo wa elimu na wanasubiri majibu kutoka kwake.
Auma aliongeza kuwa wametoa makataa ya siku 7 na wasipopata maelezo yoyote itabidi waelekee mahakamani.