Watoto wanaorandaranda mtaani mjini Mombasa wamefaidika baada ya kupata matibabu ya bure katika hafla iliyoandaliwa na kanisa la MPC kwa ushirikiano na wakfu wa Shariff Nassir.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika uwanja wa Mbaraki wakati wa hafla hiyo, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alitoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali kuangazia masuala sugu yanayoathiri wakaazi wa maeneo yao ili kuhakikisha kuwa jamii inapata usaidizi inayohitaji.

Mbunge huyo alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba familia zinazoishi mtaani zikikosa huduma muhimu za afya.

Alisema kuwa hali hiyo inatokana na familia hizo kutengwa, huku akisisitiza kuwa watoto hao wanapaswa kupewa matibabu ili kuhakikisha wana afya bora.

Kwa upande wake, Johnson Katama, mmoja wa waliofaidika na matibabu hayo alisema ni jukumu la viongozi wengine kote nchini kuiga mfano huo wa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.

Aidha, Nassir ameitaka jamii hiyo kutembelea vituo vya afya vya serikali kila mara ili kujua hali yao ya afya.