Wakaazi sasa wamelitaka Shirika la Kitaifa la Wanyama Pori (KWS) kuingilia kati na kutatua swala hilo. [Picha/howtodoright.com]

Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya punda 10 wameaga dunia baada ya kushambuliwa na fisi katika Kaunti ya Lamu.Akithibitisha kisa hicho, Felix Rachuonyo ambaye ni daktari wa mifugo, alisema kuwa visa vya punda kushambuliwa na fisi katika eneo hilo vimeongezeka.Rachuonyo alisema kuwa zaidi ya punda 40 wamebaki na majeraha mabaya baada ya kuvamiwa na fisi hao.Kwa upande wake, Bakari Bwana Ali, ambaye ni mfugaji wa punda, alisema anakadiria hasara baada ya kupoteza jumla ya punda wanne kufuatia tukio hilo la usiku wa kuamkia siku ya Jumatano."Nimepoteza punda wangu wanne ambao walikuwa ndio tegemeo langu kuu. Hii ni hasara kubwa kwangu,” alisema Bakari.Bakari sasa ameitaka Shirika la Kitaifa la Wanyama Pori (KWS) kuingilia kati na kutatua swala hilo.Alisema kuwa fisi hao wamekuwa wakiwahangaisha wafugaji hasa katika kisiwa cha Amu.“Sharti shirika la KWS litafute suluhu la kudumu la kudhibithi fisi hawa. Wanatumalizia punda wetu,” alisema Bakari.Bakari alisema kuwa huenda wakaazi wakalazimika kuchukua hatua ya kuwaua fisi hao iwapo KWS itakosa kuwajibika.Hata hivyo, Dkt Rachuonyo amewahimiza wafugaji hao kuwalinda punda wao na kuhakikisha wanalala ndani ya zizi hasa wakati wa usiku.Juhudi za mwanahabari huyu kuwapata maafisa za KWS hazikufua dafu.