Katibu wa chama cha Muungano wa Kitaifa wa Walimu nchini (KNUT) tawi la Kisii Kusini Geoffrey Mogire amewaomba wazazi kutumia sheria kuwaondoa afisini walimu wakuu wa shule mbalimbali.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wito huo umetolewa baada ya wazazi na baadhi ya wakaazi kumwondoa afisini mwalimu mkuu wa shule moja ya msingi katika eneo la Suneka kwa mabavu pasi kufuata utaratibu wa kisheria.

Mogire alisema sheria iko ya kufuatwa wakati mwalimu amekosa kwa kuripoti katika afisi za elimu kando na kutumia mabavu.

Mogire aliwakosoa wazazi na wakazi waliomuondoa mwalimu huyo afisini kwa nguvu katika eneo la Suneka na kusema huo ni ukiukaji wa sheria .

“Ikiwa mwalimu amekosa kwa kuvunja kanuni fulani sharti wazazi kutumia sheria kwa kumripoti kwa ofisi za elimu ili achukuliwe hatua na sio kutumia nguvu vile mnavyodhania,” alisema Mogire.

“Sheria iko ya kutumiwa naomba walimu na wazazi kuheshimiana na mmoja wao anapokosa anafaa kufuata sheria,” aliongeza Mogire.