Ilikuwa ni furaha na shangwe katika kitongoji duni cha Ogilgei katika eneo la Olmanyatta Kaunti Ndogo ya Subukia wakati wakaazi walipompokea mwanafunzi aliyenusurika kifo katika Chuo Kikuu cha Garissa kilicho shambuliwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.
Wakaazi hao wakiongozwa na Chifu wa Kata hiyo John Koskey pamoja na viongozi wa makanisa walionyesha furaha wazi wakishangilia kwa nyimbo na shangwe, huku mwanafunzi huyo kwa jina Alex Kibet Kirui aliye na umri wa miaka 22 akielezea jinsi alivyo epuka mauti wakati kifo kilipomkodolea macho.
“Nilishuhudia wanafunzi wenzangu wakiuwawa na magaidi. Kifo kilinikodolea macho na kwa wakati mmoja nililazimika kujifanya nimekufa kabla ya kupata mwanya wa kukimbilia usalama wangu. Lakini nashukuru Mungu kwa upendo wake na kuniepusha mauti,” alisema Kibet.
Viongozi hao ambao waliozungumza wakiwa kwenye ibada hiyo iliyofanyika katika Shule ya Upili ya Tachasis, walisema kwamba ilikuwa mapenzi yake Mungu kwa mwanafunzi huyo ambaye ni yatima na pia masomo yake yamekuwa yakifadhiliwa na wakaazi kuepuka mauti, na kumhimiza azidi kumcha Mungu na kuwasihi wakazi wafunge na kuiombea nchi.
Chief Koskey aliwataka wakaazi kufuatilia mienendo na tabia ya watoto na washirikiane na maafisa wa usalama kwa kuripoti watoto wao wanapo potea na wanapo washuku watu ambao hawana ufahamu kuwahusu.