Gavana wa Kaunti ya Tana River Hussein Dado amepuuzilia mbali madai kwamba watu kutoka maeneo mengine ya Pwani walisafirishwa katika kaunti hiyo ili wajiandikishe kama wapiga kura.
Dado alieleza kwamba huo ni uvumi usio kuwa na msingi wowote kusisitiza kuwa kamwe wakazi wa Kaunti hiyo hawafai kuukubali.
Akiongea na mwandishii huyu kwa njia ya siku siku ya Ijumma, kiongozi huyo wa kaunti alieleza kuwa wale waliosajiliwa ni watu kutoka jamii za wafugaji wa kuhamahama ambao wamekuwa katika kaunti hiyo tangu mwaka wa 2012.
“Sisi hatujasafirisha wakaazi kutoka maeneo mengine ya Pwani kuja Kaunti ya Tana River kusajiliwa kama wapiga kura. Huo ni uvumi mtupu na njama ya kuharibia sifa Kaunti ya Tana River na pia kutuharibia sisi viongozi azma yetu ya kuwania uongozi mwaka ujao,” alieleza Dado.
Aliiomba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kutenga muda zaidi ili kuendeleza usajili wa wapiga kura katika kaunti hiyo.
Itakumbukwa kuwa shughuli ya usajili wa wapiga kura kote nchini ilitamatika tarehe 15 mwezi huu.