Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua, amekashifu wafisadi waliohusika katika kupora kipande cha shamba cha makao ya wakongwe mjini Nakuru.

Akizungumza siku ya Jumatu alipotembelea makao hayo, Gavana Mbugua alisema shamba hilo lililoko eneo la Kivumbini, lilikuwa la ekari mbili lakini ekari moja ikanyakuliwa na kupatiwa mfanyibiashara wa kibinafsi.

“Serikali yangu imeanza utaratibu wa kuhakikisha kipande hicho cha ardhi kimerejeshewa wenyewe kwa kusudi la maendeleo,” alisema Gavana Mbugua.

Wakati huo huo Mbugua alisema idadi ya wakongwe pamoja na waadhiriwa wa mikasa mbali mbali inazidi kuongezeka kila kuchao.

Alisema kwamba wakongwe 50 wanaoishi katika makao hayo watapata afueni iwapo hali ya makao hayo itaimarishwa.

Gavana Mbugua alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Nakuru itatumia shilingi milioni tisa kukarabati makao hayo ya wakongwe ifikapo Januari mwaka ujao.

“Zoezi la kuwatafuta wanakandarasi watakaorabati makaazi haya tayari limekamilika,” alisema Mbugua.