Mwakilishi wa wadi ya Gesima amemtaka Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama kuwaachisha kazi wakuu wa idara wanao zembea kazini.
Atuti Nyameino alisema kuwa maafisa wengi wa serikali ya kaunti ya Nyamira ni wazembe katika kutekeleza miradi mbalimbali inayopitishwa na bunge, hali inayowafanya wananchi kupoteza imani na maafisa hao.
"Kuna wakuu wa idara huku Nyamira ambao wana mazoea yakujikokota sana katika kutekeleza miradi muhumu inayopitishwa na bunge la kaunti. Hali hiyo inawafanya wananchi kupoteza imani nasi wakidhani kwamba sisi wawakilishi wadi ndio tunaopinga maendeleo,” alisema Nyameino.
Nyameino alimhimiza Gavana Nyagarama kuwafuta kazi baadhi ya wakuu wa idara wanao zembea kazini nakuajiri wengine wapya watakao msaidia kutekeleza agenda yake ya maendeleo.
"Sisi ndio viongozi tulioko mashinani na sharti Gavana Nyagarama atusikize kwa kuwa wakuu wa idara wengi kwenye serikali yake wanazembea kazini na inafaa gavana achukue hatua yakuwaachisha kazi,” alisema Nyameino.
Mwakilishi huyo aidha alisema kuwa baadhi ya maafisa wa serikali huzembea kukagua miradi mbalimbali inayo tekelezwa na wanakandarasi hali inayo wafanya wanakandarasi hao kufanya kazi zisizo za kuridhisha.
Alisema kuwa hali hiyo husababisha pesa za umma kuvujwa.
"Baadhi ya wakuu wa idara huwa hawakagui miradi ili kutathmini utendakazi wa wanakandarasi hali inayo sababisha pesa za umma kupotea,” alisema Nyameino.