Wawakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii katika kaunti ya Kisumu, wameitisha kikao cha dharura na gavana wa Kisumu Jackton Ranguma, wakitaka kujadili maswala tofauti yanayoihusu kaunti hiyo.
Katika kikao na wanahabari jijini Kisumu mapema Jumatatu, wanaharakati hao walidai kuwepo kwa maswala kadhaa yanayopaswa kujadiliwa, kuhusiana na usimamizi wa kaunti ya Kisumu.
Walitoa makataa ya wiki moja kwa gavana kuitisha kikao hicho, huku wakitaka mawaziri kwenye serikali ya kaunti ya Kisumu kuwaeleza wananchi kuhusu utendakazi wao, na jinsi wanavyopania kufanikisha maendeleo katika jimbo la Kisumu.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza la vijana katika kaunti ya Kisumu Barnabas Odeny, wanaharakati hao wamemtaka Ranguma asitishe mara moja mizozo inayoshuhudiwa katika serikali yake.
“Tuko hapa kuitisha kikao cha umma cha mazungumzo na gavana wa Kisumu, atuelezee kuhusu utendakazi wa serikali ya kaunti ya Kisumu. Mkutano huo ni sharti uhudhuriwe pia na mawaziri wa kaunti ya Kisumu, wawakilishi wa wadi za kaunti ya Kisumu na meneja wa jiji la Kisumu miongoni mwa wengine,” alisema bwana Odeny.
Kumekuwa na malumbano ya mara kwa mara katika kaunti ya Kisumu, tangu kung’olewa madarakani kwa Spika Ann Atieno Adul mwishoni mwa mwaka jana.
Hata hivyo, Adul alirejeshwa kazini mapema mwezi huu, kufuatia agizo la mahakama ya viwanda jijini Kisumu.
Wiki jana wawakilishi wa wadi za kaunti ya Kisumu walifaa kwenda kwenye ziara jijini Nairobi, lakini ziara hiyo ikafutiliwa mbali baada ya naibu wa gavana katika kaunti ya Kisumu Ruth Odinga, kusema hakuna pesa za kufadhili ziara hiyo.