Bodi ya hospitali kuu ya mkoa PGH Nakuru sasa imemtaka Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua kueleza zilivyotumika fedha zilizonuiwa kujenga kitengo maalumu cha kujifungua cha akina mama katika hospitali hiyo.
Mwenyekiti wa bodi hiyo Samuel Githaiga katika kikao na wanahabari Jumatano mjini Nakuru alisema; "Shilingi milioni 600 zilitengwa kwa ujenzi huo kutoka serikali kuu lakini ni shilingi milioni 22 pekee ambazo serikali ya kaunti iliwasilisha kwa hospitali kuu."
Fedha hizo kwa mujibu wake, zilitengwa na serikali kuu kwa serikali ya kaunti zilifaa kuwasilisha kwa hospitali kuu kuwezesha ujenzi huo. Alidai kuwa huenda kuna baadhi ya maafisa wa kaunti waliotumia vibaya fedha hizo.
Ni kutokana jambo hilo ambapo Githaiga alisisitiza kuwa kama bodi ya hospitali ya PGH hawatanyamaza wakati fedha zinavujwa.
"Ufisadi ndio adui wa maendeleo na hatutanyamaza wakati fedha zinatumiwa kwa njia isiyofaa,"aliongeza Githaiga.
Juhudi za mwanahabari huyu kumfikia waziri wa afya kaunti ya Nakuru Dr Mungai Kabii hazikufua dafu kwani hakupokea simu.