Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ametia sahihi kwa makubaliano na shirika moja lisilo la kiserikali kwa jina Power Hive ili kuwapa umeme wakaazi wa Kaunti hiyo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Shirika hilo litawasaidia wakaazi wa Kaunti hiyo kupata nguvu za umeme baada ya wengi wa wakaazi hao kutokuwa na uwezo wa kuunganishiwa nguvu hizo za umeme kwa muda mrefu.

Akizungumza afisini mwake iliyoko mjini Nyamira alipokuwa na Maafisa wa shirika hilo siku ya Ijumaa, Gavana Nyagarama  alipongeza shirika hilo na kusema kuwa wakaazi wa Kaunti hiyo watanufaika pakubwa na mradi huo baada ya kutokuwa na nguvu za umeme makwao maana hugharimu pesa nyingi.

Shirika hilo la Power Hive limesema kuwa watawalipisha wakaazi hao Sh3,500 pekee ili kupata nguvu hizo za umeme.

Wakati uo huo, Gavana Nyagarama alisema kuwa Kaunti yake haitalipa shirika hilo chochote ila kuwapa sehemu ya kuweka makao yao jinsi shirika hilo lilihitaji.

“Wakaazi wanaotaka umeme watahitajika kulipa Sh3,500 pekee ili waunganishiwe nguvu za umeme na hiyo si kulipa bali ni kugharamia nyaya zinazotumika kuunganisha nguvu hizo,” alisema Gavana Nyagarama.

Kwa upande mwingine, wakaazi hao wa Kaunti hiyo ya Nyamira walifurahishwa na mradi huo na kusema watajaribu wawezalo kutafuta hizo pesa zinazohitajika ili kupata nguvu hizo za umeme.

“Nimefurahi sana na mradi huu wa nguvu za umeme na niko tayari kulipa hizo pesa hata siku ya leo, bora nipate nguvu hizo,” alihoji Lawrence Nyagaka mkaazi.