Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewafadhili wanafunzi 32 wa Shule ya Upili ya Rigoma godoro 60 na Sh100,000 ili wanunuliwe vitabu na sare za shule.

Share news tips with us here at Hivisasa

Shule hiyo iliyoko katika Wadi ya Rigoma eneo Bunge la Kitutu Masaba Kaunti ya Nyamira ilishika moto siku ya Jumapili asubuhi na kuchoma vitabu na sare za shule za wanafunzi hao 32, jambo lilimpelekea gavana huyo kuwafadhili wanafunzi hao godoro 32, blanketi na Sh100,000 pesa taslimu ili wananunue bidhaa walizopoteza kwenye kisa hicho.

Akizungumza siku ya Jumanne katika shule hiyo ya Rigoma, Gavana Nyagarama alisema serikali yake iliamua kuwafadhili wanafunzi hao ili kurejelea masomo yao kama kawaida na kupokea elimu ambayo itawasaidia siku zijazo.

“Serikali yangu iliona ni busara tuwakumbuke wanafunzi hawa waliokumbwa na hasara wakati mkasa wa moto ulishika bweni ya wanafunzi hawa na kuwapelekea kupata hasara,” alisema Gavana Nyagarama.

“Wanafunzi wanapaswa kuendelee na masomo yao bila taswishi yoyote maanake vitabu na sare mlizozipoteza sasa zitanunuliwa Serikali ya Kaunti ya Nyamira inahitaji viwango vya masomo kuinuka juu zaidi, na hicho kinawezekana tu mkiwa mnasoma bila tatizo lolote,” aliongezea Nyagarama.

Wakati uo huo, wanafunzi walifurahishwa na usaidizi huo na kumshukuru Gavana Nyagarama kwa kuwakumbuka ili kurejelea mosomo yao kama kawaida.

“Mimi nilikuwa tayari nimepoteza imani maana sikuwa na mahala pa kuanzia kufuatia bidhaa zangu zilizochomeka. Mungu amlinde gavana wetu na tunasema asante,” alihoji Morine Obiero mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyekumbwa na mkasa huo.