Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Kaunti ya Tana River Hussein Dado ameitaka serikali kuu kuzitengea kaunti fedha zaidi ili kuimarisha sekta mbalimbali zinazokumbwa na uhaba wa fedha.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa kaunti za pwani mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Dado alisema kwamba sekta ya elimu, uchukuzi na miundo msingi zinastahili kupewa kipau mbele ili kuona kwamba wakazi wanafaidika pakubwa na serikali za ugatuzi.

"Tungependa kuona serikali inaongeza fedha zaidi katika kaunti ili tuweze kuwafanyia wakazi maendeleo kwa sababu pesa wanazotupatia ni kidogo mno,” alisema Dado.

Kulingana na Dado, japo serikali za kaunti za pwani zimejitahidi kujenga zaidi ya madarasa 75 ya shule za chekechea na kuajiri wahudumu 301 wa shule hizo, bado kuna mahitaji zaidi wakazi wanahitaji kufanyiwa.

Dado aliwahimiza wakazi wa kaunti za pwani kuzidi kudumisha amani kwa kuwa na uiano na utangamano miongoni mwa jamii, huku akiwatahadharisha dhidi ya kutumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa na kuvurugana.

Gavana huyo aliahidi kuimarisha uhusiano wema baina ya wakazi na viongozi wa kaunti ili kuona kwamba maswala ya maendeleo yanatekelezwa sambamba na kuwasaidia wakazi wanapokumbwa na chnagamoto.