Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wikendi hii ilikuwa ya furaha kwa baadhi ya watoto wa shule ya chekechea mjini Mombasa, walioshiriki mashindano ya pamoja yaliyohudhuriwa na viongozi wakuu katika kaunti, akiwemo Gavana Hassan Joho.

Takriban shule tisa kutoka maeneo mbalimbali mjini humo zilishiriki mashindano hayo yaliyoandaliwa katika Shule ya chekechea ya Burhaniya siku ya Jumamosi.

Mashindano hayo yalikuwa na lengo la kuwaleta pamoja watoto wadogo, pamoja na kutumia njia hiyo kama mbinu ya kutambua vipaji vyao mapema.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho aliyeongoza viongozi wengine katika tamasha hilo alifurahishwa na hatua hiyo na kuahidi kuendelea kuunga mkono mashindano hayo ili kukuza vipaji vya watoto.

“Tutazidi kuunga mkono michezo kama hii ili tuone kwamba watoto wanakua katika kufahamu michezo mbalimbali na pia kukuza talanta katika eneo letu la Mombasa,” alisema Gavana Joho.

Viongozi wengine walioandamana na Gavana Joho katika hafla hiyo ni pamoja na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir miongoni mwa wengine.