Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema tangu uchaguzi mdogo wa Malindi ulipokamilika, amekuwa akipitia masaibu mengi huku biashara zake zikilengwa zaidi.
Joho alisema kuwa biashara zake zilianza kuandamwa mwezi mmoja uliopita lakini masaibu yake yalizidi tangu chama cha ODM kiliposhinda huko Malindi.
Aidha, Gavana Joho ameitaka serikali kumpa heshima kama kiongozi aliyechaguliwa kikatiba na kusisitiza kwamba katiba inaruhusu upinzani kutekeleza majukumu yake bila kushurutishwa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu, Gavana Joho alisema licha ya kwamba serikali inamtaka kurejesha bunduki zake, bado hajapewa taarifa maalum, huku akimlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani Joseph Nkaissery kwa kutumia vyombo vya habari kuzungumzia swala hilo.
“Waziri Nkaissery pamoja na Marwa wameamua kuzungumzia hili swala kupitia vyombo vya habari bila ya kutumia njia zinazofaa, lakini mimi nitafuata utaratibu wa kisheria kusuluhisha haya mambo,” alisema Joho.
Wakati huo huo, Gavana Joho alisema kuwa kuna dhulma nyingi zilitendeka wakati wa uchaguzi mdogo wa Malindi lakini serikali ya Jubilee imekataa kuangazia swala hilo huku ikitumia njia za ujanja kuziba aibu hiyo.
Joho amemlaumu mshirikishi wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa akisema kuwa anahusika pakubwa na masaibu anayopitia, huku akiongeza kuwa serikali ilimpokonya walinzi na kumlazimisha kurejesha bunduki ili kuziba aibu.
“Nitasalia kuwa kiongozi mwaminifu kwa wananchi na wala siwezi kusaliti chama cha ODM na hakuna vitisho vitakavyoniyumbisha kamwe,” alisema Joho.
Kauli ya Gavana Joho inajiri huku waziri wa usalama wa ndani akisisitiza kwamba anafaa kurejesha bunduki yake kwa serikali.